Sunday, April 3, 2016

Kimeta chaua mmoja, 197 wachunguzwa



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadik.
 
MTU mmoja amefariki kwa ugonjwa wa kimeta wilayani Rombo, huku wengine 197 wakiwa katika uangalizi maalumu na wanne wakitambulika kuugua baada ya kula nyama yenye vimelea vya ugonjwa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema ugonjwa huo umeripotiwa katika vijiji vya Ubetu, Wama na Kilongo na wagonjwa wanaendelea na matibabu katika Hospitali Teule ya Huruma.

Sadiki ambaye alifanya ziara katika wilaya hiyo, aliagiza wananchi kutokula nyama za wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe bila kuthibitishwa na wataalamu wa afya ili kuepusha kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.


Taarifa ya Sadiki iliyotumwa jana na Ofisa Habari wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaban Pazi, ilieleza kuwa kuna uwezekano wa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro na tayari chanjo kwa mifugo inaendelea.

Alitaka wataalamu wa sekta ya afya kudhibiti uhamishwaji wa mifugo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hususan maeneo ya mipakani na nchi ya Kenya ili kuhakikisha mifugo ya nchini inayopata chanjo haipati maambukizi mengine ya ugonjwa huo.

Serengeti Boys yang’ra



Wachezaji wa Serengeti Boys wakishangilia bao la pili dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana ya Misri (The Pharaohs) chini miaka 17 katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki uliochezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Serengeti ilishinda mabao 2-1. (Picha na Yusuf Badi).

TIMU ya soka ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, jana ilipata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Misri, katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo ni ishara njema kwa klabu ya Yanga ambayo wiki ijayo itaikabili Al Ahly, kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini pia kwa timu ya taifa ya wakubwa ‘Taifa Stars’ ambayo mwezi Juni, itaikabili Misri, katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika ‘Afcon’.
Hadi mapumziko Serengeti Boys, inayonolewa na kocha Bakari Shime, ilikuwa mbele kwa bao moja lililofungwa na kiungo Cyprian Benedictor, aliyewalamba chenga mabeki wanne wa Misri na kumtungua kipa Amro Boghdady.

Kipindi cha pili Misri walionekana kuja juu baada ya kufanya mabadiliko kwa kuwaingiza Mahmud Mohamed na Mohamed Hegaze, kuchukua nafasi za Mohamed Elsayed na Walid Ataia na jitihada zao zilizaa matunda dakika 85 baada ya Diaa Wahed kuisawazishia timu yake kwa shuti kali.

Kuingia kwa bao hilo kuliwazindua Serengeti ambao waliutawala kwa asilimia kubwa mchezo huo na kufanya mashambulizi mengi kwenye lango la Misri, lakini umaliziaji ulikuwa butu.

Wakati mashabiki wakiamini mchezo ungemalizika kwa sare, beki wa kati, Ally Hussein, aliifungia Serengeti Boys, bao la ushindi dakika ya 90, baada ya kupanda mbele na kupokea krosi ya Boko Selemani.

Saturday, April 2, 2016

M’kiti halmashauri Arusha, wenzake 4 kortini kwa tuhuma za kujeruhi






MWENYEKITI wa Halmashauri ya Arusha, Noah Lembris

 
MWENYEKITI wa Halmashauri ya Arusha, Noah Lembris na wenzake wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za kujeruhi na kuharibu mali.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Gwanta Mwankuga na kusomewa mashtaka yanayowakabili katika kesi namba 83 na 84 za mwaka 2016 .

Pamoja na Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ambaye ni Diwani wa Kata ya Oltumet kupitia Chadema, watuhumiwa wengine ni William Samwel, Rafael Ngosira, Loserian Solomon na Lucas Lairumbe.

Akisoma mashtaka hayo, Mwanasheria wa Serikali Riziki Riziki alidai mahakamani hapo kuwa mshatakiwa wa kwanza Noah Lembris na Wiliam Samweli kwa pamoja Septemba 27, mwaka jana katika eneo la Olorien wilayani Arumeru walidaiwa kuchoma moto nyumba ya mkazi wa eneo hilo Peter Kambey.

Katika shtaka la pili linalowakabili watuhumiwa wote inadaiwa Februari 29, mwaka huu wanadaiwa kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili Peter Kambey wakati akiwa shambani kwake na kumsababishia maumivu makali.

Watuhumiwa wote walikana mashtaka yanayowakabili na waliachiwa kwa dhamana hadi Aprili 14, mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo. Awali kabla ya kupandishwa mahakamani na kusomewa mashtaka hayo, watuhumiwa hao walikuwa katika mgogoro wa kugombea shamba lenye ukubwa wa ekari 6 mali ya ajuza Ndetiai Megaro (84) mkazi wa kijiji cha Ilkiushi wilayani Arumeru.

Mgogoro huo uliodumu kwa takriban miaka 12 unatokana na baadhi ya viongozi wa kisiasa akiwemo Mwenyekiti Lembris kujaribu kudhulumu shamba hilo kwa kuhamisha umiliki kutoka kwa bibi huyo na kudai kuwa ni eneo la kijiji cha Ilkiushi.

Kitilya, wenzake wawili kortini




Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (wa pili kushoto), Shose Sinare (wa pili kulia) na Sioi Sumari (kushoto) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana. (Na Mpigapica Wetu).


SAKATA la rushwa ya Dola za Marekani milioni 600, linalohusisha Benki ya Standard ya London Uingereza, jana lilichukua sura mpya baada ya kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, akikabiliwa na mashitaka mbalimbali, ikiwemo utakatishaji wa fedha.

Washitakiwa wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni pamoja na mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon. Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni 6, sawa na Sh bilioni 12 za Tanzania.

Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Emilius Mchauru washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande mpaka Aprili 8 mwaka huu, wakati mahakama itakapokutana kusikiliza shauri kuhusu dhamana yao. Upande wa utetezi, ukiwakilishwa na mawakili Dk Ringo Tenga na Semu Anney, waliomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wao.

Hata hivyo, upande wa Mashitaka ukiwakilishwa na wanasheria waandamizi wa Serikali; Oswald Tibabyekomya na Christopher Msigwa pamoja na Mwanasheria wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Stanley Luwoga walipinga dhamana hiyo kwa madai kuwa kesi za utakatishaji fedha hazina dhamana.

Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama kwamba, katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013, katika Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.

Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, mshitakiwa Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ikiwa na tarehe ya Agosti 2, 2012.

Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia 2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.

Mahakama ilielezwa kuwa Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa Tanzania, aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Imedai kuwa Septemba 20, 2012 katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza barua ya uongo ya kuelezea mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza kuwa Benki ya Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic, zitatoa mkopo huo kwa Serikali kama wakikubaliwa
.
Upande huo wa mashitaka uliendelea kudai kuwa, Sinare aliwasilisha barua hiyo ya uongo katika Wizara ya Fedha kwa lengo hilo hilo. Kwa mujibu wa madai hayo, Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia ovu, walitengeneza makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki imeipa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited, kazi ya kushughulikia mkopo huo.

Bei ya umeme yashuka

 
 
MAMLAKA ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imepunguza bei ya umeme baada ya kupokea ombi la Shirika la Umeme (Tanesco). Katika maombi yake, Tanesco waliomba kupunguza umeme kwa asilimia 1.1 lakini baada ya Ewura kupitia maombi hayo imepunguza kwa asilimia 1.5 hadi 2.4 kutoka bei ya sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei hiyo mpya ya umeme, imeanza kutumika jana. Kwa mujibu wa Ngamlagosi, Ewura walifikia hatua hiyo ya kupunguza zaidi ya maombi ya Tanesco, baada ya kukaa na wadau.
Mbali na kushusha bei ya umeme, Ngamlagosi alisema pia baadhi ya gharama ambazo ni tozo ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme ambayo ilikuwa Sh 5,000 na tozo ya huduma ya mwezi (service charge) iliyokuwa Sh 5,520 kwa wateja wa majumbani ambao wapo katika kundi la T1, pia vimefutwa Ngamlagosi alisema hata marekebisho ya bei za umeme kwa mwaka 2017, yameahirisha mpaka Tanesco itakapowasilisha upya maombi hayo kabla ya Agosti 31, mwaka huu.
“Kutokana na kifungu cha Sheria ya Umeme ya mwaka 2008, kifungu cha 23 (2) na 23 (3), yatakuwepo marekebisho ya bei za umeme kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta, thamani ya fedha na mfumuko wa bei. Marekebisho hayo yatafanyika kwa mujibu wa kanuni ya 7 ya urekebishaji wa bei za umeme ya mwaka 2016,” alisema.

Aliongeza kuwa kundi la wateja wadogo wa nyumbani wale wa kipato kidogo ambao wanatumia uniti moja hadi 75, wanatakiwa kwa mwezi kulipa Sh 350 kwa kila uniti inayozidi.

Pia, kwa watu wa majumbani wenye matumizi makubwa wana punguzo la Sh 6 kutoka Sh 298 kwa uniti hadi 292. Kundi jingine lililonufaika na punguzo hilo, limetajwa kuwa ni wafanyabiashara wa kati ambao ni wenye mitambo, hoteli na migahawa ambao wana punguzo la Sh 5 kutoka Sh 200 hadi 195.

Ngamlagosi alifafanua kuwa wateja wa viwandani wamepunguziwa Sh 2 kwa uniti toka Sh 159 hadi 157 na wateja wanaotumia msongo mkubwa wa umeme wana punguzo la Sh 4 kutoka Sh 156 hadi 152 kwa uniti.

Alisema pia Tanesco ilipeleka ombi la punguzo la umeme la mwaka 2017 ambalo walipendekeza bei ya umeme ipungue kwa asilimia 7.9, lakini pendekezo hilo limeahirishwa mpaka hapo watakapowasilisha upya maombi kabla ya Agosti 31, mwaka huu.

Mkwasa arejea Yanga




Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwassa.
 
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa ameitwa kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la Yanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri wiki ijayo.

Habari zilizopatikana jana kutoka Yanga, zilieleza kuwa tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshatoa ruhusa ili aweze kuisaidia Yanga kipindi hiki cha kuelekea mchezo huo. “Ni kweli Mkwasa ameitwa kuongeza nguvu, unajua Kocha wa Yanga (Hans Pluijm), anamkubali sana Mkwasa, hivyo wameona aje asaidie wakati huu ambapo hana majukumu Taifa Stars,” kilisema chanzo chetu na kusisitiza kwamba Mkwasa haina maana amejiondoa Taifa Stars.

Mkwasa hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, wala Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro na hata Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto. Hata hivyo, TFF iliwahi kutoa taarifa kwamba timu za Yanga na Azam zipo huru kuwatumia makocha wa Taifa Stars, Mkwasa na Hemed Morocco katika maandalizi yao kwa ajili ya michezo ya kimataifa inayowakabili.

Mkwassa alikuwa Kocha Msaidizi wa Yanga kabla ya kuteuliwa kuwa kocha muda wa Taifa Stars katikati ya mwaka uliopita akirithi mikoba ya Mholanzi Mart Nooij aliyetimuliwa baada ya matokeo mabaya ya Stars.

TFF ilisaini naye mkataba wa miezi 18 Oktoba mwaka jana baada ya kuridhishwa na kazi yake, ambapo mkataba huo utamalizika Machi 31 mwakani. Wakati huohuo, Mohammed Akida anaripoti kuwa Pluijm amesema ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC juzi utachangia kukiimarisha kikosi chake kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly mwishoni mwa wiki ijayo.
Yanga juzi ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho, lakini haikuonesha kiwango cha kuvutia kiasi cha mashabiki kuingiwa na hofu kuhusu mchezo wao na Ahly.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Pluijm alikiri timu yake kucheza vibaya, lakini alisema hiyo ni moja ya mikakati yao kuhakikisha wanatunza nguvu za kucheza mechi zingine tatu zinazowakabili ikiwemo ya Al Ahly.

Pluijm alisema huo ni ushindi mkubwa kwao na sasa wanajipanga kushinda michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kabla ya kuikabili Al Ahly Jumamosi ijayo.

Friday, April 1, 2016

Usawa wa kijinsia katika jamii za kitanzania bado ni kizungumkuti




 


Wanafunzi wakisikiliza semina
 
 Bi Fatma Amiry akitoa semina ya jinsia katika ukumbi wa chuo cha uandishi wa habari Arusha

Kulingana na usanyanyasaji wa kijinsia unaoendelea katika maeneo  mbalimbali  nchini,jamii imehaswa kuweka usawa wa kijinsia ili kuweza kutokomeza adha hiyo.
Hayo yamesemwa na  Bi. Fatma Amiry ambaye ni Afisa ustawi wa jamii mkoani Arusha  katika semina  ya  kupinga unyanyasaji  wa kijinsia na maambukizi ya Ukimwi iliyofanyika katika ukummbi wa chuo cha Uandishi wa Habari na utangazaji  Arusha (AJTC).
Ameeleza kuwa  jamii  nyingi  za kitanzania bado zinamitazamo  hasi kuhusiana na suala la usawa  wa kijinsia  kutokana na mila na destuuri walizojiwekea  ambazo  zinaleta migogoro na usnyanyasaji wa kijinsia.
Bi Fatma amesema  jamii inatakiwa ibadilike kulingana na wakati uliopo ili kuweza kuleta usawa huo katika jamii ikiwa ni pamoja na wanawake kurithi mali,kupewa elimu na kutokudharauliwa
“Ni wakati wa mabadiliko katika jamii zetu, maisha ya zamani ni tofauti na sasa hivyo nawaomba watanzania wenzangu waache kunyanyasa jinsia tofauti ili kuweza kutimiza malengo ya haki sawa kwa wote”Alisema Bi. Fatma Amiry
Licha ya hayo pia amewashauri vijana na jamii kwa ujumla  kupima afya  na kuwa  waaminifu kwa wapenzi wao  ili kuweza kupunguza kasi ya maambukizi  ya  virus vya  Ukimwi
Kwa upande wake mkufunzi wa chuo hicho Bw. Lucas Modaha amesema  vijana na wanandoa wajiheshimu na kulinda utu ili kuepuka maambukizi mapya ya VVU