Thursday, March 31, 2016

MWANZA KINARA WATUMISHI HEWA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene

WAKUU wa mikoa 26 ya Tanzania Bara wamekabidhi ripoti za uhakiki wa watumishi hewa katika mikoa yao, ambazo zimeonesha kuwa na watumishi hewa zaidi ya 2,000, huku Mkoa wa Shinyanga ukiwa hauna mtumishi hewa yeyote wakati Mwanza ndio kinara ukiwa na watumishi hewa 334.

Watumishi hao zaidi ya 2,000 wameisababishia serikali hasara zaidi ya Sh bilioni nne, huku mikoa ya Mwanza, Singida, Kigoma, Pwani, Dodoma, Morogoro na Kilimanjaro ikionekana kuwa na idadi kubwa ya watumishi hewa.

Ripoti hizo ziliwasilishwa jijini Dar es Salaam jana na Wakuu wa Mikoa hao kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye alisema ripoti hizo atazifikisha kwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi kwa ajili ya kuhakikiwa, kabla ya kuwasilisha kwa Rais John Magufuli.

“Nitazipeleka kwa Waziri wa Utumishi ili yeye azifanyie uhakiki na zipitiwe upya…hata kwenye wizara pia ufanywe uhakiki wa watumishi hewa kwa sababu unaweza ukakuta hata wizarani wapo. Hili suala nitalifikisha kwa Waziri wa Utumishi,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa baada ya kukamilika itafikishwa mbele ya Rais Magufuli.

Aidha, aliwataka wakuu hao wa mikoa, kutambua mamlaka yao na kuyatumia ipasavyo ili kila aliyehusika kwa namna moja au nyingine katika watumishi hao hewa anachukuliwa hatua haraka ipasavyo. Awali, wakiwasilisha ripoti zao, baadhi ya wakuu wa mikoa walisema kuwa bado hawajapata idadi kamili ya fedha zilizopotea kutokana na idadi ya watumishi hewa katika mikoa yao.

Akiwasilisha ripoti yake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Daudi Ntibenda alisema wamebaini kuwepo kwa watumishi hewa 270 ambao wamesababisha hasara ya Sh bilioni 1.8 katika kipindi cha mwaka mmoja. Wengine waliowasilisha na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella (334). Alisema bado hawajapata idadi halisi ya hasara kutokana na watumishi hao kulipwa mishahara.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mathew Mtigume aliwasilisha (231) na hawajapata gharama halisi za fedha walizochota. Mikoa mingine iliyowasilisha ripoti na idadi ya watumishi hewa kwenye mabano ni Kigoma (171) hasara Sh milioni 104.6, Pwani (150) hasara bado haijapatikana, Dodoma (139) hasara ni Sh milioni 287 kwa kipindi cha miezi sita, Morogoro (122) hasara ni zaidi ya Sh milioni 450, Kilimanjaro (111) hasara Sh milioni 281.4
.
Mingine ni Tanga (104) hasara bado haijapatikana, Mbeya na Songwe (98) hasara ni Sh milioni 459.6, Mara (94) hasara Sh milioni 121, Dar es Salaam (73) hasara Sh milioni 316, Lindi (57) hasara Sh milioni 36.2, Tabora (38) hasara Sh milioni 118.7 na Ruvuma (37) hasara Sh milioni 58. Mkoa wa Simiyu (62) hasara Sh milioni 320, Njombe (34) hasara Sh milioni 20.1, Katavi (21) hasara Sh milioni 20.7, Manyara (50) hasara Sh milioni 42, Iringa (15) hasara haijapatikana na Kagera (14) hasara Sh milioni 49.1.

Akitoa siri ya mkoa wake kutokuwa na watumishi hewa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela alisema viongozi waliotangulia kabla yake, waliweka mikakati mizuri jambo lililowezesha wasiwepo watumishi hao. “Viongozi waliokuwepo walianza zoezi hili tangu mwezi Julai mwaka jana na kila tarehe 26 ya mwisho wa mwezi walikuwa wakihakiki watumishi wao hivyo ndio maana hakuna watumishi hewa,” alisema Anne- Kilango, ambaye katika Serikali ya Awamu ya Nne alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri alisema katika mkoa wake yapo majina ya watumishi hewa, ambayo yapo katika orodha ya malipo ya mishahara, na kutoa mfano wa Manispaa ya Tabora peke yake hasara iliyotokana na kulipa watumishi hewa ni Sh milioni 24. Machi 15, mwaka huu wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa, Rais Magufuli alitoa siku 15 kwa viongozi hao kuhakikisha wanajumuisha wafanyakazi wote na kuwaondoa watumishi hewa.

Aidha, juzi Rais Magufuli alisema uhakiki mdogo uliofanywa hivi karibuni kuhusu tatizo la wafanyakazi hewa nchini, umebaini wafanyakazi hewa 1,680 waliokuwa wakilipwa Sh bilioni 1.8. Alisema ni matarajio kuwa uhakiki unaofanywa nchi nzima, utaisaidia serikali kubaini wafanyakazi hewa wengi zaidi na kunusuru fedha nyingi zaidi za Watanzania.

Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Chato mkoani Geita juzi, Rais Magufuli alitoa mfano wa mfanyakazi mmoja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambaye alikuwa akilipwa mishahara ya watu 17, na kueleza kuwa mfanyakazi huyo atafikishwa mahakamani. Awali akifungua kikao cha kujadili bajeti inayopelekwa bungeni na utekelezaji wa bajeti iliyopita, Waziri Simbachawene aliwaagiza Wakuu wa Mikoa hao kuhakikisha wanasimamia vizuri elimu bila malipo.

“Lakini pia hakikisheni watumishi wanajituma na kuwafundisha wanafunzi vizuri ili kupata elimu bora. Kuna malalamiko mengi ya wananchi ambayo yanafika mpaka kwa Rais na baadaye ndio yanarudi kwa waziri na mkuu wa mkoa, tujitahidi kuhakikisha tunatatua migogoro katika hatua ya mwanzo,” alisema Simbachawene.
Aidha, aliwaagiza kushughulikia tatizo la mlundikano wa watumishi katika maeneo ya mijini kwani mlundikano huo hauna tofauti na watumishi hewa. Alisema kwa kada ya ualimu zipo shule ambazo zina idadi kubwa ya walimu kuliko mahitaji.

“Unakuta shule moja walimu wanaotakiwa ni 40 tu lakini unakuta 120 hadi wengine hawana kazi…kisingizio ni kwamba hela ya uhamisho wahamisheni sisi tutatoa hela ya uhamisho,” alisema Simbachawene. “Serikali za Mitaa katika maeneo yenu zizingatie kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, serikali imejipanga kuhakikisha inapunguza gharama za kujiendesha kwa kubana matumizi katika maeneo yasiyokuwa na tija,” aliongeza Simbachawene.
 
“Mamlaka zote zinasimamia jambo la ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha ukusanyaji huo unafanyika kwa njia ya elektroniki, ambao unaonesha matokeo mazuri ni lazima uwe umeunganishwa katika mfumo wetu kwa sababu wapo watu wana zile mashine lakini hazijaungwa katika mfumo wetu,” alisema.

UPIMAJI WA MAENEO YA KILIMO NA UFUGAJI YAANZA KWA KASI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

KATIKA kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuona hatua zinachukuliwa za kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, kazi ya kupima maeneo ili kutenganisha matumizi ya kilimo na ufugaji imeanza kwa kasi.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, ilipotembelea ofisi za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA), ambayo imeanza kufanya kazi hiyo katika vijiji mbalimbali nchini.

Akiwaapisha Wakuu wa Mikoa hivi karibuni, Rais Magufuli alisema sababu kubwa iliyomfanya kumuondoa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe ilikuwa ni kwa kiongozi huyo kushindwa kukomesha mapigano baina ya wakulima na wafugaji yaliyoshamiri mkoani humo.

Mratibu wa Mkurabita, Seraphia Mgembe akitoa maelezo mbele ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Dk Pudensiana Kikwembe (CCM), alisema upimaji wa maeneo ya ardhi ni moja ya manufaa ya Mpango wa Mkurabita kwa Taifa.

“Ndugu Makamu Mwenyekiti uwepo wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 96 umechangia kupunguza migogoro ya ardhi katika vijiji hivyo. “Katika maeneo yote tuliyopima tumefanikiwa kukomesha migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa kuoanisha maeneo ambayo ni kwa ajili ya wakulima tu na maeneo ambayo ni kwa ajili ya wafugaji tu, na wananchi wenyewe ndio wanaotusaidia katika kufikia uamuzi huo ambao unaheshimiwa na pande zote,” alisema Mgembe.

Pamoja na faida hiyo, Mratibu huyo alisema urasimishaji wa ardhi na biashara unaofanywa na Mkurabita pia umewezesha wamiliki 208 waliopewa Hati za Haki Miliki za kimila, kutumia hati hizo kama dhamana na kupata mikopo ya thamani ya Sh bilioni 2.4 na wakati huo huo vyama vitano vya wakulima vimepata mkopo wenye thamani ya Sh bilioni 4.7
.
 Kwa upande wa mjini, alisema wamiliki 93 waliorasimisha viwanja vyao mjini wametumia hati miliki zao kupata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.07

Monday, March 28, 2016

Shein aitisha Baraza la Wawakilishi



 

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ameitisha mkutano wa kwanza wa Baraza jipya la Tisa la Wawakilishi keshokutwa kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani mjini Unguja.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Dk Yahya Khamis Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi jana.

Hamad alisema amepokea barua kutoka kwa Rais Shein ambayo inaitisha mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi, ambalo kwa mujibu wa kanuni zake, linamtambua Rais kama ni sehemu ya pili ya baraza hilo na ndiyo mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na mahala pa kufanyika mkutano wa kwanza.

Alisema kama Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2012 linaelezea kuwa katika Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wawakilishi shughuli ya mwanzo ni kumchagua Spika wa Baraza la Wawakilishi, na hadi sasa aliyeteuliwa na kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ambaye amethibitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Zuber Ali Maulid kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu wa Baraza la Wawakilishi alisema wajumbe wote wameanza kujengewa mazoea ikiwa pamoja na kujisajili kuanzia leo hadi Aprili 6, mwaka huu. “Kesho (leo) kusajiliwa kwa wajumbe na kupigwa picha za vitambulisho, Machi 29 asubuhi kutakuwa na mkutano wa vyama vya siasa, pia siku hiyo mchana kutakuwa na mkutano wa mwanzo wa wajumbe wote wa baraza, Machi 30 kuanza kwa mkutano wa kwanza wa baraza na baadaye uchaguzi wa spika pamoja na kiapo cha spika na wajumbe,” alisema Hamad.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Machi 31, mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa Naibu Spika na Mwenyekiti wa Baraza, Aprili 5, 2016 kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe wa Tume ya Bajeti ya Baraza na wajumbe watano wa baraza watakaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baraza hilo jipya linalotarajiwa kuanza keshokutwa litakalohutubiwa na Dk Shein lina idadi ya wajumbe 88 ambao wajumbe 54 ni wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, 22 Wawakilishi wa Viti Maalumu, 10 uteuzi wa Rais ambao bado kuteuliwa, Mjumbe mmoja ambaye ni Mwanasheria Mkuu na Spika ambaye ni nje ya wajumbe wa baraza.

Shein aitisha Baraza la Wawakilishi



 

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein ameitisha mkutano wa kwanza wa Baraza jipya la Tisa la Wawakilishi keshokutwa kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi, Chukwani mjini Unguja.
Hayo yameelezwa na Katibu wa Baraza la Wawakilishi, Dk Yahya Khamis Hamad wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Baraza la Wawakilishi jana.

Hamad alisema amepokea barua kutoka kwa Rais Shein ambayo inaitisha mkutano wa kwanza wa Baraza la Wawakilishi, ambalo kwa mujibu wa kanuni zake, linamtambua Rais kama ni sehemu ya pili ya baraza hilo na ndiyo mwenye mamlaka ya kuamua tarehe na mahala pa kufanyika mkutano wa kwanza.

Alisema kama Kanuni za Baraza la Wawakilishi Toleo la 2012 linaelezea kuwa katika Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Wawakilishi shughuli ya mwanzo ni kumchagua Spika wa Baraza la Wawakilishi, na hadi sasa aliyeteuliwa na kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo ambaye amethibitishwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar ni Zuber Ali Maulid kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Katibu wa Baraza la Wawakilishi alisema wajumbe wote wameanza kujengewa mazoea ikiwa pamoja na kujisajili kuanzia leo hadi Aprili 6, mwaka huu. “Kesho (leo) kusajiliwa kwa wajumbe na kupigwa picha za vitambulisho, Machi 29 asubuhi kutakuwa na mkutano wa vyama vya siasa, pia siku hiyo mchana kutakuwa na mkutano wa mwanzo wa wajumbe wote wa baraza, Machi 30 kuanza kwa mkutano wa kwanza wa baraza na baadaye uchaguzi wa spika pamoja na kiapo cha spika na wajumbe,” alisema Hamad.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa Machi 31, mwaka huu kutakuwa na uchaguzi wa Naibu Spika na Mwenyekiti wa Baraza, Aprili 5, 2016 kutakuwa na uchaguzi wa wajumbe wa Tume ya Bajeti ya Baraza na wajumbe watano wa baraza watakaoingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Baraza hilo jipya linalotarajiwa kuanza keshokutwa litakalohutubiwa na Dk Shein lina idadi ya wajumbe 88 ambao wajumbe 54 ni wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, 22 Wawakilishi wa Viti Maalumu, 10 uteuzi wa Rais ambao bado kuteuliwa, Mjumbe mmoja ambaye ni Mwanasheria Mkuu na Spika ambaye ni nje ya wajumbe wa baraza.

Dk Magufuli: Tusibaguane





RAIS John Magufuli amewataka Watanzania waendeleze upendo na mshikamano walionao ili kuendelea kuilinda amani ya nchi na wasibaguane. Akizungumza wakati wa Ibada ya Pasaka iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) la Azania Front, Dar es Salaam jana, Rais Magufuli alisema Watanzania wanapaswa kutokubaguana kwa dini, rangi wala makabila na washirikiane katika umoja wao.

Rais Magufuli alisema wakati taifa likiadhimisha sikukuu hiyo ya kufufuka kwa Yesu Kristo, wananchi wanapaswa kusherehekea kwa kufanya kazi ili taifa lisonge mbele.
“Niwaombe Watanzania wenzangu wakati tunaadhimisha Sikukuu hii ya kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo tufufuke naye katika upendo wake lakini tufanye kazi kweli kweli kwa sababu vitabu vinasema asiyefanya kazi na asile,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, alisema endapo Watanzania kwa umoja wao wakiamua kufanya kazi kwa bidii, Taifa halitakuwa masikini na kuacha kutegemea misaada ya wahisani wa nje. Alisema kuwa Tanzania ni nchi iliyojaaliwa neema kwa kuwa na rasilimali nyingi na hivyo wananchi wanatakiwa kusimama imara ili iweze kuja kuwa Taifa litakalokuwa likitoa misaada kwa mataifa mengine ya nje.

Rais Magufuli aliwaomba Watanzania kutochoka kuliombea Taifa pamoja na yeye ambaye ana jukumu gumu na zito lakini kupitia maombi ya wananchi anaamini atatimiza yale aliyotakiwa kuyatimiza.

“Naomba Watanzania tusichoke kuliombea Taifa letu, na mimi nawashukuru kwa kuendelea kuniombea. Jukumu hili ni gumu, zito na ni msalaba lakini najua kwa sala zenu, kwa maombi yenu nitatimiza yale ninayotakiwa kuyatimiza,” alieleza Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliyeongoza ibada hiyo, aliwakumbusha wananchi kurejesha maadili ndani ya nyumba zao yaliyoanza kupotea kwa kumrudia Mungu.

Askofu Malasusa alisema kuwa fmilia nyingi siku hizi zimeparaganyika, ndoa nyingi zimekuwa hazidumu kwa sababu watu wameacha kufanya ibada na hivyo maadili tena katika nyumba yamepotea. “Tufufue maisha ya uadilifu ndani ya ndoa zetu.

Siku hizi baba na mama wanazikimbia nyumba zao kwa sababu maadili yamepotea ndani ya nyumba, turudishe maadili kwa kufanya ibada,” alisema Dk Malasusa. Aidha, Askofu Malasusa aliwataka Watanzania kwa imani zao kuacha kumsifu Rais Magufuli kwa kupiga makofi na badala yake kila mmoja kwa imani yake asimame na kumuombea kwa kuwa sasa taifa limeanza kuwa na matumaini mapya na nuru kwa kumpata kiongozi aliye mwadilifu.

Saturday, March 12, 2016

Katibu Mtendaji NACTE ajiuzulu


KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dk Primus Nkwera.

KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), Dk Primus Nkwera, amejiuzulu nafasi hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali. Uamuzi wa kujiuzulu kwa Dk Nkwera, ulitangazwa juzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Baraza hilo, Steven Mlote wakati akizungumza na wafanyakazi wa baraza hilo kwenye kikao cha dharura

Mlote alisema, Dk Nkwera amefikia uamuzi wa kujiuzulu, ili kulinda hadhi ya baraza hilo, baada ya gazeti moja la kila wiki kuchapisha habari zikimtuhumu kwa mambo mbalimbali, ikiwemo madai ya kughushi vyeti.
Alisema kwa mujibu wa Dk Nkwera nafasi kubwa kama hiyo katika taasisi ya elimu, haipaswi kushikwa na mtu mwenye tuhuma ya aina yoyote, hivyo baada ya kutafakari ameona ajiweke pembeni na uongozi wa baraza hilo, ili uchunguzi ufanyike akiwa pembeni.

“Tumetumia muda mrefu kutafakari hoja za Dk Nkwera na tumekubali kujiuzulu kwake kwa shingo upande,” alisema Mlote akiwaambia wafanyakazi waliokuwa katika kikao hicho. Mlote alisema kazi iliyofanywa na Dk Nkwera akiwa kiongozi wa baraza hilo inafahamika kwa kila mmoja na uamuzi wake huo ni majonzi kwa baraza hilo.

“Najua mmepata mshituko mkubwa, lakini Dk Nkwera hajafa. Yuko hai, na huyu bado ni mtumishi wa Serikali. Alichofanya ni kuamua kuachana na ukatibu mtendaji. Tutaendelea kumtumia itakapobidi kwa ushauri.

“Wakati mwingine ni lazima mkubaliane na hali hii, lakini endeleeni kuchapa kazi kwa ufanisi kama kawaida, kana kwamba bado mko na Dk Nkwera,” alisema Mlote. Kutokana na kujiuzulu kwa Dk Nkwera, Mlote alieleza kuwa Bodi imemteua Mkurugenzi wa Mitaala wa baraza hilo, Dk Adolf Rutayunga kukaimu nafasi hiyo wakati taratibu nyingine zikiendelea.
Akizungumza katika kikao hicho, Dk Rutayunga alisema kuwa viatu ambavyo ameiacha Dk Nkwera ni vikubwa kwake lakini atajitahidi kuhakikisha anaendeleza yale yote ambayo ameyaacha.
“Jambo hili ni kubwa, uamuzi huu wa kujiuzulu kwa Dk Nkwera ni mzito, lakini hatuna cha kufanya. Tutashikamana kuhakikisha kwamba kazi za Baraza zinasonga mbele kwa weledi uleule” alisema.
Mlote alipotafutwa na mwandishi wetu alikiri Dk Nkwera kujiuzulu bila kueleza kwa undani sababu za kujiuzulu kwake. “Ni kweli amejiuzulu nafasi yake, lakini siwezi kukupa maelezo yote kwa sababu niko barabarani naendesha gari,” alisema Mlote

Wafukiwa wakiiba madini Mirerani



 
WACHIMBAJI wadogo watatu wanasadikiwa kufa baada ya kufukiwa na kifusi, wakati wakiwa kwenye harakati za kuiba madini ya tanzanite katika mgodi wa Tanzanite One, Mirerani.
Taarifa ya kufukiwa kwa wachimbaji hao maarufu kama Wanaapolo, ilitolewa jana na mchimbaji mwenzao, Gidish Benedict (32), aliyekuwepo eneo la tukio na kunusurika wakati wenzake wakifukiwa.
Kwa mujibu wa Benedict aliyezungumza na waandishi wa habari mjini hapa, hajui kama wenzake watakuwa hai, kwani sehemu waliyokuwepo haikuwa na hewa hivyo kuna uwezekano wa wenzake watatu kufa wakiwa huko chini.
Aliwataja wenzake hao waliofukiwa kuwa ni Saidi Mgosi, mkazi wa Boma mkoani Kilimanjaro na wengine aliowataja kwa jina moja kuwa ni Dominic, mkazi wa Zaire Mirerani kwa jina la utani anaitwa Bwashee na Khalid, ambaye hafahamu anakotoka.
“Sijui kama wenzangu wapo hai au la maana nilimwambia mbona nguzo imebana sana, wakasema toka wewe si mzoefu wacha sisi wazoefu tufanye kazi. “Nilijibanza pembeni ya mwamba na kuwapisha watengeneze njia ili tutoke, lakini wakati wakigonga nguzo, udongo ulimwagika kwa kasi mimi nikarudi kwenye upenyo nikafanikiwa kupona, lakini sijui wenzangu kama wapo hai watakuwa wamefukiwa na kifusi,” alisema.
Amekiri kuwa walizama ndani ya mgodi huo Jumatatu ya wiki hii saa 7 usiku kwa njia za panya maarufu ‘bomu’, lakini wenzake wamefukiwa na kifusi na haijulikani kama wako salama.
*Tanzanite One
Akizungumzia jana Mirerani, Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Sky Associates, inayomiliki mgodi huo wa Tanzanite One, Apolinary Modest alisema Wanaapolo hao waliingia katika mgodi huo uliofungwa Jumatatu wiki hii na kuanza kuchimba madini.
Kwa mujibu wa Modest, baada ya kumaliza kazi hiyo walianza safari ya kurudi juu, lakini walishindwa kufika juu siku ya Ijumaa, baada ya kugonga nguzo ambayo ilitoa udongo mwingine uliosababisha njia hiyo ya panya kuziba.
“Hivi sasa tupo na wataalamu wetu wa uokoaji kutoka Afrika Kusini kwa ajili ya kuwaokoa Wanaapolo hawa ambao hatujui kama wapo hai au la. “Bado kama mita mbili au tatu kufika eneo la tukio chini ya ardhi ili kuona kama wapo hai au wamekufa au wamepita njia nyingine za panya na kukimbia,” alisema Modest.
Alisema njia za panya zipo nyingi na kampuni imejitahidi kuziba, lazini zinazibuliwa na Wanaapolo ili kuingia ndani ya mgodi uliofungwa au unaoendelea kuchimbwa madini hayo kwa nia ya kuiba madini.
Modest alisema machimbo yapo mengi zaidi ya 100 ambayo yamezibwa, lakini Wanaapolo hao wamekuwa wakizibua kwa njia zao na kuingia eneo la Tanzanite One, ili kuiba madini hayo na mchimbaji huyo aliye hai, anashirikiana na waokoaji kuonesha njia walizopita ili wenzake waokolewe.
Wanaowapeleka Shuhuda huyo, Benedict aliendelea kusema kazi hiyo ya kwenda kuiba madini, hufadhiliwa na wafanyabishara wakubwa wa madini ambao hutoa mamilioni ya fedha kwa wachimbaji hao ili wafanikishe wizi huo.
Alisema wao hawana nia mbaya, bali husukumwa na wafanyabiashara hao ambao hutenga mamilioni ya fedha kwa kazi hiyo. ‘’Sisi tunanunuliwa zana zote za uchimbaji na tunatumwa kwenda kuiba madini Tanzanite One na huko chini ni usalama wako ndio unakulinda na ukipata madini, unampelekea kwa aliyekufadhili ambaye ni mafanyabiashara mkubwa wa tanzanite.
“Naomba mnisamehe maana msukumo ndio unatufanya tufanye kazi hii ya bomu na njaa pia inachangia,’’ alisema. Kamanda wa Polisi wilayani Simanjiro, Francis Massawe amethibitisha tukio hilo na kuongeza kuwa bado wanaendelea na uokozi. Imeandikwa na Veronica Mheta na John Mhala, Arusha.