Thursday, March 31, 2016

UPIMAJI WA MAENEO YA KILIMO NA UFUGAJI YAANZA KWA KASI

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

KATIKA kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuona hatua zinachukuliwa za kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, kazi ya kupima maeneo ili kutenganisha matumizi ya kilimo na ufugaji imeanza kwa kasi.

Hayo yalibainishwa Dar es Salaam jana wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, ilipotembelea ofisi za Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge (MKURABITA), ambayo imeanza kufanya kazi hiyo katika vijiji mbalimbali nchini.

Akiwaapisha Wakuu wa Mikoa hivi karibuni, Rais Magufuli alisema sababu kubwa iliyomfanya kumuondoa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe ilikuwa ni kwa kiongozi huyo kushindwa kukomesha mapigano baina ya wakulima na wafugaji yaliyoshamiri mkoani humo.

Mratibu wa Mkurabita, Seraphia Mgembe akitoa maelezo mbele ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake, Mbunge wa Jimbo la Kavuu, Dk Pudensiana Kikwembe (CCM), alisema upimaji wa maeneo ya ardhi ni moja ya manufaa ya Mpango wa Mkurabita kwa Taifa.

“Ndugu Makamu Mwenyekiti uwepo wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 96 umechangia kupunguza migogoro ya ardhi katika vijiji hivyo. “Katika maeneo yote tuliyopima tumefanikiwa kukomesha migogoro baina ya wakulima na wafugaji kwa kuoanisha maeneo ambayo ni kwa ajili ya wakulima tu na maeneo ambayo ni kwa ajili ya wafugaji tu, na wananchi wenyewe ndio wanaotusaidia katika kufikia uamuzi huo ambao unaheshimiwa na pande zote,” alisema Mgembe.

Pamoja na faida hiyo, Mratibu huyo alisema urasimishaji wa ardhi na biashara unaofanywa na Mkurabita pia umewezesha wamiliki 208 waliopewa Hati za Haki Miliki za kimila, kutumia hati hizo kama dhamana na kupata mikopo ya thamani ya Sh bilioni 2.4 na wakati huo huo vyama vitano vya wakulima vimepata mkopo wenye thamani ya Sh bilioni 4.7
.
 Kwa upande wa mjini, alisema wamiliki 93 waliorasimisha viwanja vyao mjini wametumia hati miliki zao kupata mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.07

No comments:

Post a Comment