Waziri wa ujenzi na mawasiliano profesa Makame Mbarawa |
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, ametoa mwezi mmoja kwa watu na taasisi zilizokopa nyumba za Serikali kulipa. Mbarawa aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumza na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Alisema anataka fedha hizo zilipwe haraka, vinginevyo atawataja katika vyombo vya habari watakaoshindwa kukamilisha madeni yao na kuagiza waondoke kwenye nyumba hizo. “Kama ni watu binafsi au taasisi za Serikali ni lazima walipe ili na sisi tuendelee kufanya kazi zetu vizuri.
Naomba mlisimamie hilo na fedha hizo zilipwe,” Mbarawa alisema. Aliongeza kuwa huu ni wakati wa kufanya kazi kwa kasi inayostahili. Profesa Mbarawa alisema pia kuwa ufisadi katika wizara hiyo sasa ni mwiko. Alisema kuwa ufisadi hauangalii ukubwa wala udogo hivyo kwake uwe mdogo au mkubwa ni ufisadi tu.
“Ninajua na ninyi TBA mna kashfa zenu. Ninawaambia tutapambana na wajanja wajanja wote kwa sababu hatutaki tufike katika majipu,” alisema. Aidha, aliwataka wafanyakazi wa wakala huo kufanya kazi kwa weledi na kuacha kufika ofisini ‘kuchati’ katika mitandao ya kijamii na kuondoka, badala ya kufanya kazi.
Wakati huo huo, alitoa onyo kwa wanaotumia namba zake za simu kufanya utapeli na kusema atawachukulia hatua za kisheria
No comments:
Post a Comment