Saturday, April 2, 2016

Bei ya umeme yashuka

 
 
MAMLAKA ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imepunguza bei ya umeme baada ya kupokea ombi la Shirika la Umeme (Tanesco). Katika maombi yake, Tanesco waliomba kupunguza umeme kwa asilimia 1.1 lakini baada ya Ewura kupitia maombi hayo imepunguza kwa asilimia 1.5 hadi 2.4 kutoka bei ya sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema bei hiyo mpya ya umeme, imeanza kutumika jana. Kwa mujibu wa Ngamlagosi, Ewura walifikia hatua hiyo ya kupunguza zaidi ya maombi ya Tanesco, baada ya kukaa na wadau.
Mbali na kushusha bei ya umeme, Ngamlagosi alisema pia baadhi ya gharama ambazo ni tozo ya kuwasilisha maombi ya kuunganishiwa umeme ambayo ilikuwa Sh 5,000 na tozo ya huduma ya mwezi (service charge) iliyokuwa Sh 5,520 kwa wateja wa majumbani ambao wapo katika kundi la T1, pia vimefutwa Ngamlagosi alisema hata marekebisho ya bei za umeme kwa mwaka 2017, yameahirisha mpaka Tanesco itakapowasilisha upya maombi hayo kabla ya Agosti 31, mwaka huu.
“Kutokana na kifungu cha Sheria ya Umeme ya mwaka 2008, kifungu cha 23 (2) na 23 (3), yatakuwepo marekebisho ya bei za umeme kutokana na mabadiliko ya bei za mafuta, thamani ya fedha na mfumuko wa bei. Marekebisho hayo yatafanyika kwa mujibu wa kanuni ya 7 ya urekebishaji wa bei za umeme ya mwaka 2016,” alisema.

Aliongeza kuwa kundi la wateja wadogo wa nyumbani wale wa kipato kidogo ambao wanatumia uniti moja hadi 75, wanatakiwa kwa mwezi kulipa Sh 350 kwa kila uniti inayozidi.

Pia, kwa watu wa majumbani wenye matumizi makubwa wana punguzo la Sh 6 kutoka Sh 298 kwa uniti hadi 292. Kundi jingine lililonufaika na punguzo hilo, limetajwa kuwa ni wafanyabiashara wa kati ambao ni wenye mitambo, hoteli na migahawa ambao wana punguzo la Sh 5 kutoka Sh 200 hadi 195.

Ngamlagosi alifafanua kuwa wateja wa viwandani wamepunguziwa Sh 2 kwa uniti toka Sh 159 hadi 157 na wateja wanaotumia msongo mkubwa wa umeme wana punguzo la Sh 4 kutoka Sh 156 hadi 152 kwa uniti.

Alisema pia Tanesco ilipeleka ombi la punguzo la umeme la mwaka 2017 ambalo walipendekeza bei ya umeme ipungue kwa asilimia 7.9, lakini pendekezo hilo limeahirishwa mpaka hapo watakapowasilisha upya maombi kabla ya Agosti 31, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment