Saturday, April 2, 2016

Kitilya, wenzake wawili kortini




Kamishna Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya (wa pili kushoto), Shose Sinare (wa pili kulia) na Sioi Sumari (kushoto) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana. (Na Mpigapica Wetu).


SAKATA la rushwa ya Dola za Marekani milioni 600, linalohusisha Benki ya Standard ya London Uingereza, jana lilichukua sura mpya baada ya kufikishwa mahakamani kwa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, akikabiliwa na mashitaka mbalimbali, ikiwemo utakatishaji wa fedha.

Washitakiwa wengine waliounganishwa katika kesi hiyo ni pamoja na mrembo wa zamani wa Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sheria wa benki hiyo, Sioi Graham Solomon. Mashitaka mengine yanayowakabili katika kesi hiyo mbali na kutakatisha fedha, ni pamoja kutumia nyaraka za kughushi na za uongo kujipatia isivyo halali Dola za Marekani milioni 6, sawa na Sh bilioni 12 za Tanzania.

Mbele ya Hakimu Mwandamizi, Emilius Mchauru washitakiwa hao walikana mashitaka hayo na kurudishwa rumande mpaka Aprili 8 mwaka huu, wakati mahakama itakapokutana kusikiliza shauri kuhusu dhamana yao. Upande wa utetezi, ukiwakilishwa na mawakili Dk Ringo Tenga na Semu Anney, waliomba mahakama itoe dhamana kwa wateja wao.

Hata hivyo, upande wa Mashitaka ukiwakilishwa na wanasheria waandamizi wa Serikali; Oswald Tibabyekomya na Christopher Msigwa pamoja na Mwanasheria wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Stanley Luwoga walipinga dhamana hiyo kwa madai kuwa kesi za utakatishaji fedha hazina dhamana.

Awali upande wa mashitaka uliieleza mahakama kwamba, katika tarehe tofauti kati ya Agosti 2012 na Machi 2013, katika Jiji la Dar es Salaam, washitakiwa hao watatu walipanga pamoja kwa kushirikiana na watu wengine ambao hawakufikishwa mahakamani hapo, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa udanganyifu kutoka serikalini.

Ilidaiwa kuwa kati ya Agosti 2, 2012 katika Makao Makuu ya Benki ya Stanbic Tanzania Limited yaliyopo wilayani Kinondoni, mshitakiwa Sinare akiwa na nia ovu, alighushi taarifa ya maombi ya fedha ya Benki ya Standard ikiwa na tarehe ya Agosti 2, 2012.

Kwa mujibu wa madai hayo, Sinare alieleza katika maombi hayo kuwa Benki ya Standard ya London kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic ya Tanzania, watatoa mkopo unaofikia Dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa gharama ya asilimia 2.4 ya mkopo huo, wakati akijua kuwa gharama hiyo si kweli.

Mahakama ilielezwa kuwa Agosti 13, 2012, mrembo huyo wa zamani wa Tanzania, aliwasilisha taarifa hiyo ya kughushi katika Wizara ya Fedha iliyopo Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Imedai kuwa Septemba 20, 2012 katika Benki ya Stanbic, Sinare alitengeneza barua ya uongo ya kuelezea mkopo huo wa Dola za Marekani milioni 550, ikieleza kuwa Benki ya Standard PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic, zitatoa mkopo huo kwa Serikali kama wakikubaliwa
.
Upande huo wa mashitaka uliendelea kudai kuwa, Sinare aliwasilisha barua hiyo ya uongo katika Wizara ya Fedha kwa lengo hilo hilo. Kwa mujibu wa madai hayo, Novemba 5, 2012 katika Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam, washitakiwa wote watatu, wakiwa na nia ovu, walitengeneza makubaliano ya uongo kwa lengo la kuonesha kuwa benki imeipa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors (EGMA) Limited, kazi ya kushughulikia mkopo huo.

No comments:

Post a Comment