Tuesday, April 12, 2016

MKUTANO BOMBA WA MAFUTA WAANZA UGANDA










RAIS WA UGANDA YOWERI KAGUTA MUSEVENI
MKUTANO unaohusu ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Uganda hadi Bahari ya Hindi, umeanza mjini Kampala nchini Uganda. Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), mkutano huo, ulianza jana, unashirikisha mataifa waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ni Kenya, Uganda na Tanzania na baada ya siku tatu maofisa wa Serikali kutoka mataifa hayo wataamua.
Maofisa hao wataamua iwapo bomba hilo linafaa kutoka Uganda na kupitia nchini Tanzania hadi Bandari ya Tanga au kupitia Kenya hadi Bandari ya Lamu au Bandari ya Mombasa.
Bomba la kutoka Tanga hadi Uganda, litakuwa na urefu wa kilometa 1,410 na litasafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima eneo la Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Bomba la kutoka Hoima na kwenda Lokichar kisha hadi Lamu, linakuwa na urefu wa kilomita 1,476 jambo ambalo linainyima Kenya fursa ya bomba hilo kujengwa nchini humo.
Pendekezo la kutoa mafuta Lokichar kisha kupitia Hoima nchini Uganda na kufika Tanga, itakuwa na urefu wa kilomita 2,028. Ingawa ripoti itakayojadiliwa imetoa njia tatu zinazoweza kutumiwa, ni dhahiri kuwa Kenya na Tanzania watakuwa katika hali ya kuchunguzana zaidi kuhusu jambo hilo.
Mazungumzo ya mwezi mmoja uliopita kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Rais Yoweri Museveni na wakati huo huo kati ya Rais Museveni tena na Rais John Magufuli juu ya suala la bomba la kupeleka mafuta hadi Bahari ya Hindi, yamezusha uhasama baridi kati ya Kenya na Tanzania.
Tayari vyombo vya habari nchini Tanzania, vimesema kuwa Rais Magufuli na Rais Museveni walishafikia makubaliano ya bomba hilo lipitie Tanzania hadi Bandari ya Tanga.
Mkutano uliofanyika nchini Kenya kati ya Rais Kenyatta na Rais Museveni juu ya bomba hilo, kufuatia mwaliko wa Rais Kenyatta, ulimalizika wiki chache zilizopita bila suluhu yoyote.
Kenya na Tanzania kila nchi ingependa kuona bomba la mafuta, linapitia kwake kutokana na manufaa ya kiuchumi. Mafuta ghafi ya Kenya hayako mbali na yale ya Uganda, lakini ni wazi kwamba kuwa na bomba nchini ni biashara ya kipekee inayoleta faida zaidi.

No comments:

Post a Comment