Sunday, April 3, 2016

Kimeta chaua mmoja, 197 wachunguzwa



Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadik.
 
MTU mmoja amefariki kwa ugonjwa wa kimeta wilayani Rombo, huku wengine 197 wakiwa katika uangalizi maalumu na wanne wakitambulika kuugua baada ya kula nyama yenye vimelea vya ugonjwa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki amesema ugonjwa huo umeripotiwa katika vijiji vya Ubetu, Wama na Kilongo na wagonjwa wanaendelea na matibabu katika Hospitali Teule ya Huruma.

Sadiki ambaye alifanya ziara katika wilaya hiyo, aliagiza wananchi kutokula nyama za wanyama kama ng’ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe bila kuthibitishwa na wataalamu wa afya ili kuepusha kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.


Taarifa ya Sadiki iliyotumwa jana na Ofisa Habari wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaban Pazi, ilieleza kuwa kuna uwezekano wa kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro na tayari chanjo kwa mifugo inaendelea.

Alitaka wataalamu wa sekta ya afya kudhibiti uhamishwaji wa mifugo kutoka sehemu moja kwenda nyingine, hususan maeneo ya mipakani na nchi ya Kenya ili kuhakikisha mifugo ya nchini inayopata chanjo haipati maambukizi mengine ya ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment