Saturday, April 2, 2016

Mkwasa arejea Yanga




Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwassa.
 
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Mkwasa ameitwa kuongeza nguvu katika benchi la ufundi la Yanga kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri wiki ijayo.

Habari zilizopatikana jana kutoka Yanga, zilieleza kuwa tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeshatoa ruhusa ili aweze kuisaidia Yanga kipindi hiki cha kuelekea mchezo huo. “Ni kweli Mkwasa ameitwa kuongeza nguvu, unajua Kocha wa Yanga (Hans Pluijm), anamkubali sana Mkwasa, hivyo wameona aje asaidie wakati huu ambapo hana majukumu Taifa Stars,” kilisema chanzo chetu na kusisitiza kwamba Mkwasa haina maana amejiondoa Taifa Stars.

Mkwasa hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, wala Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro na hata Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto. Hata hivyo, TFF iliwahi kutoa taarifa kwamba timu za Yanga na Azam zipo huru kuwatumia makocha wa Taifa Stars, Mkwasa na Hemed Morocco katika maandalizi yao kwa ajili ya michezo ya kimataifa inayowakabili.

Mkwassa alikuwa Kocha Msaidizi wa Yanga kabla ya kuteuliwa kuwa kocha muda wa Taifa Stars katikati ya mwaka uliopita akirithi mikoba ya Mholanzi Mart Nooij aliyetimuliwa baada ya matokeo mabaya ya Stars.

TFF ilisaini naye mkataba wa miezi 18 Oktoba mwaka jana baada ya kuridhishwa na kazi yake, ambapo mkataba huo utamalizika Machi 31 mwakani. Wakati huohuo, Mohammed Akida anaripoti kuwa Pluijm amesema ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ndanda FC juzi utachangia kukiimarisha kikosi chake kwa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly mwishoni mwa wiki ijayo.
Yanga juzi ilishinda mabao 2-1 katika mchezo wa robo fainali Kombe la Shirikisho, lakini haikuonesha kiwango cha kuvutia kiasi cha mashabiki kuingiwa na hofu kuhusu mchezo wao na Ahly.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Pluijm alikiri timu yake kucheza vibaya, lakini alisema hiyo ni moja ya mikakati yao kuhakikisha wanatunza nguvu za kucheza mechi zingine tatu zinazowakabili ikiwemo ya Al Ahly.

Pluijm alisema huo ni ushindi mkubwa kwao na sasa wanajipanga kushinda michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kabla ya kuikabili Al Ahly Jumamosi ijayo.

No comments:

Post a Comment