WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) anafanya uhakiki wa madeni ya watumishi wanayoidai serikali ambayo imebainika kuwapo madudu.
Alisema madai mengine yameonesha mashaka hivyo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wakuu wa ndani kujiridhisha ukweli wake kabla ya kuyafikisha serikalini kwa ajili ya malipo.
Majaliwa alisema hayo juzi wakati akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa alipotembelea hospitalini hapo akiwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukabidhi msaada wa vifaa tiba alivyovitoa kwa ajili ya hospitali hiyo
.
“Madai mengine yanatia mashaka, sisi hatuhitaji kuletewa madeni ya hovyo hovyo, ni vema Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakaguzi wa ndani wakajiridhisha kabla ya kuyapeleka serikalini kwa ajili ya malipo,” alisema.
Alitoa mfano wa madeni aliyoyaita ya ajabu, akisema, “unakuta mtumishi mmoja anaidai serikali Sh milioni 30, jambo ambalo ni gumu hata kama alihamishwa, haiwezekani kufikia kiwango hicho. Pia kuna baadhi ya majina yamejirudia mara nne.
”
Alisema serikali italipa madeni yote inayodaiwa baada ya kumaliza kuyafanyia uhakiki. Aliomba watumishi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na uhakiki iweze kulipa deni sahihi.
Awali , akisoma taarifa ya Idara ya Afya kwa Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Dk Japhet Simeo alisema Idara ya Afya inakabiliwa na madeni ya watumishi ambayo ni Sh milioni 109.6 Alisema madeni hayo yametokana na likizo, matibabu, uhamisho wa ndani na nje ya wilaya, gharama za mizigo kwa watumishi waliostaafu.
Alisema halmashauri imejipangia utaratibu wa kulipa madeni hayo itakapopata fedha kutoka serikali kuu. Dk Simeo alimpongeza Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Majaliwa kwa juhudi kubwa wanazofanya kuongeza mapato nchini.
No comments:
Post a Comment