Tuesday, February 23, 2016


Bilioni 4/- zaokolewa kwa kuzuia safari


Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi, George Simbachawene
OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeokoa Sh bilioni 4.38 ambazo zingetumika na watumishi wa Halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya safari za ndani.
Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene alibainisha hayo katika kipindi maalumu cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano kinachorushwa na kituo cha televisheni cha TBC1 cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
“Katika kipindi cha siku 95, tumeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo watumishi wa halmashauri wangezitumia katika safari za ndani zisizo na tija na hazijalenga kumkomboa mwananchi huyu ambaye hana dawa na hana barabara,” alisema Simbachawene.
Akizungumzia uwajibikaji wa watumishi katika halmashauri nchini, Simbachawene alisema ili kuhakikisha halmashauri hizo zinafanya kazi ipasavyo, wameunda kitengo cha ukaguzi ambacho kina kazi ya kudhibiti na kufuatilia utendaji wa kazi za halmashauri.
“Tamisemi tuna deni kubwa, kwani sisi ndio tunaotegemewa na wizara kutafsiri mipango yao ya elimu afya, miundombinu na sekta nyingine. Tamisemi ni wakala wa serikali kwa wananchi,” alisema na kuongeza kuwa watendaji wa halmashauri ambao hawataki kwenda na kasi ya Rais Magufuli, basi wataondolewa katika nafasi zao bila kuonewa haya.
“Tutahakikisha tunawachukulia hatua wezi wote, wabadhirifu na wasio waadilifu, huwezi utupishe. Tutawapima kwa jinsi wanavyoondoa kero kwa wananchi,” alisema na kukiri kuwa katika halmashauri kuna matatizo ya uadilifu jambo linalofanya miradi mingi kushindwa kukamilika na ikikamilika inakuwa chini ya kiwango.
Aidha, amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanawafikia wananchi na kumaliza kero za wananchi kinyume chake kazi wataiona chungu.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato, Simbachawene alisema asilimia 95 ya halmashauri zote zimeanza kutumia mfumo wa elektroniki katika kukusanya mapato na kuwa zile chache ambazo hazijaanza zimetakiwa kufanya hivyo baada ya kuongezewa muda kidogo

No comments:

Post a Comment